SHIDA ni sehemu ya maisha ya binadamu. Katika dunia hii kuna wakati maisha hujaribu kuleta kila aina ya masumbuko na kama hutasimama katika mstari imara ni rahisi kushindwa na hatimaye kuanguka kabisa
Kila kitu huonekana kwenda kombo, na baadhi yetu hufikia hatua ya kukata tamaa na kuamua kuyaacha mambo yaende kama yaliyo, kwa kusema eti Mungu ndiye kapenda iwe vile, kitu ambacho si sahihi kabisa.
Wakati mwingine ili uweze kusimama katika misingi imara kimaisha, basi ni lazima ukutane na vizingiti, dhoruba na vikwazo ikiwa ni moja kati ya njia za kukukomaza kimaisha.
Kuna vitu vikuu viwili maishani ambavyo mtu hawezi kuepukana navyo kwa namna yoyote ile, navyo ni Furaha na Huzuni. Hivi ni vitu ambavyo kila mtu huvipitia, lakini cha kushangaza, watu wengi sana hupenda kukutana na furaha na inapokuja hali ya maumivu, basi wengi wetu hunyong’onyea na kuwa dhaifu katika utendaji wa mambo.
Yafuatayo ni badhi ya mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa pindi mtu unapokutana na nyakati ngumu:-
1️⃣Kubaliana na hali halisi
Pindi unapokuwa unakabiliana na wakati mgumu maishani mwako, usikimbilie kukata tamaa, hatua ya kwanza kufanya ni kukubaliana na ukweli wa hali yenyewe ilivyokupata.
Kamwe hiki si kipindi cha kulaumu, hata kama wewe ndiyo chanzo cha tatizo hilo, bado hupaswi kujilaumu kwa kile ulichokifanya. Lakini pia usilipe nafasi kubwa tatizo hilo katika akili yako, kwani kufanya hivyo ni kuzidi kulikuza unachotakiwa ni kuwa mtulivu ili uweze kutafuta njia ya kulitatua.
2️⃣Usimweleze kila mtu hali unayopitia
Watu wengi hukosa uvumilivu pindi wanapokuwa katika nyakati ngumu na kujikuta wakigeuka waropokaji kwa kila mtu wakidhani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutatua matatizo yao, jambo ambalo si kweli.
Pamoja na ukweli kwamba matatizo huhitaji msaada wa kimawazo kutoka kwa watu wengine lakini si kwa kila mmoja unayekutana naye au kumuona. Jaribu kuwafuata baadhi ya watu ambao unaamini kuwa wanaweza kuleta suluhu, ukimweleza kila mtu ni rahisi kupata ushauri wa kukuvunja moyo.
3️⃣Usikae bila kujishughulisha.
Muda wote unapopitia wakati mgumu usipende sana kukaa bila kujishughulisha kiakili na kimwili kila wakati ili kuitokomeza hali ya huzuni na maumivu unayokabiliana nayo. Pendelea kufanya baadhi ya vitu vinavyoweza kukuletea faraja na furaha, mfano labda kujisomea baadhi ya maandiko yatakayokupa mwanga, fanya mazoezi, angalia hata mechi mbalimbali za mpira pamoja na mambo ambayo unaamini ukiyafanya utapata mwelekeo mpya kimtazamo.
4️⃣Epuka mfadhaiko.
Unapopitia wakati mgumu haupaswi kabisa kukaa peke yako muda mrefu, kwani kwa kufanya hivi unakaribisha mfadhaiko akilini mwako kutokana na ugumu wa kimaisha unaokutana nao. Changamana na makundi ya watu wenye furaha ili wakusaidie kuponya huzuni yako.
5️⃣Jiamini na utumie uwezo wako wote.
Ndani yako kuna uwezo mkubwa sana ambao ukiutumia kikamilifu, unaweza kutatua baadhi ya mambo bila hata ya kuhitaji msaada kwa mtu mwingine. Unapaswa kujiamini. Usiwe na mashaka na uwezo ulionao ndani yako. Tambua maisha ni safari na dereva wake ni wewe mwenyewe.
6️⃣Usikate tamaa.
Katika maisha watu wengi hukwama kutatua changamoto zao si kwa sababu hawana uwezo la, ila ni ile hali ya kukata tamaa mapema inapowakumba.
Kwenye maisha hakuna kukata tamaa, hata kama hali ni ngumu kiasi gani usikubali kushindwa, endelea kupambana hadi tone la mwisho la jasho lako litakapoanguka ardhini, ari hii ni silaha kubwa sana ya kufanikiwa katika kupata furaha unayoitafuta.
7️⃣Kubali kubaki na Mungu.
Kiuhalisia katika wakati ambao mwanadamu hubaki na Mungu wake pekee ni pale anapopitia nyakati ngumu, kipindi hiki ndipo mtu huwa na toba ya kweli na majuto ya dhati, kipindi hiki mtu humkosa hata yule aliyekuwa wa karibu yake. Nyakati ngumu humsogeza mwanadamu kwa Mungu.
8️⃣Paza sauti ya ushindi.
Watu wengi wanapokuwa kwenye hali ngumu za kimaisha hudhani kuwa kila kitu kitakuwa hivyo milele. Unapoishi kama mtu hai ni lazima upitie kila aina ya hali ngumu lakini ni vyema ukaamini kuwa kila kitu kina mwisho wake, kwenye kila hali ngumu mtangulize Mungu, paza sauti ya ushindi itoke moyoni mwako, kila mara jitangazie kuwa hili nalo litapita kama lilivyoweza kupita lile.